Steve Ballmer mmoja wa maofisa wa Kampuni ya Microsoft |
Kampuni maarufu inayotengeneza
programu za kompyuta, Microsoft, itanunua sehemu muhimu ya biashara ya kampuni
ya kutengeneza simu za mkononi Nokia kwa kiasi cha euro bilioni 5.44. Katika
tangazo la pamoja la makampuni hayo mawili juma hili, ilielezwa kuwa Microsoft
itanunua kitengo cha huduma vifaa na huduma cha Nokia kwa euro bilioni 3.79, na
pia hati miliki au hataza ya kampuni hiyo kwa euro bilioni 1.62.
Katika makubaliano hayo,
Microsoft itakuwa na haki ya kutumia huduma ya ramani ya kampuni ya Nokia.
Makubaliano hayo, ambayo kwa mujibu wa wadau wake yatapanua mipaka ya
mawasiliano ya simu za mkononi, yatakamilishwa mwanzoni mwa mwaka ujao.
Katika makubaliano hayo, wafanyakazi
32,000 wa Nokia watahamia katika kampuni ya Microsoft. Aidha, makubaliano hayo
yanamweka mkurugenzi mkuu wa Nokia Stephen Elop katika nafasi nzuri ya kuchukua
nafasi itakayoachwa wazi na mkuu wa Microsoft Steve Ballmer ambaye atastaafu mwaka
kesho.