Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeendelea kuzitaka kampuni za simu nchini humo kulipa tozo ya shilingi 1000 kila mwezi kwa laini moja ya simu ndani ya siku 14.
Awali tozo hiyo ilitakiwa kuanza kulipwa julai mwaka huu lakini kutokana na malalamiko ya wadau,utekelezaji huo ulisubiri mapendekezo ya Tume Maalumu iliyoundwa na Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete kushughulikia suala hilo.
Hivi karibuni umoja wa wamiliki wa Kampuni za simu nchini Tanzania (MOAT) ulisema asilimia 48 ya watanzania ndio wanaotumia simu za mkononi sawa na watu milioni 22.
Kutokana na tozo hiyo inakadiliwa kuwa zaidi ya asilimia 40 hadi 45 watafungiwa simu zao na kudai takribani watanzania milioni nane hushindwa kuweka shilingi 1000 kwa mwezi katika laini zao za simu.
Tume iliyoundwa na Rais Kikwete kushughulikia suala hilo ilijumuisha wajumbe kutoka TRA,Wizara ya Fedha na wawakilishi wa kampuni za simu.
Julai 19 mwaka huu,Waziri wa Fedha,Dkt William Mgimwa alisema serikali imekubali kupitia mawazo na maoni ya MOAT kuhusu kufutwa kwa tozo hiyo ambayo imelalamikiwa na wadau wengi wa sekta ya mawasiliano.