Tuesday, April 1, 2014

SERIKALI YA TANZANA YAWATAHADHARISHA WANANCHI KUZINGATIA MATUMIZI SAHIHI YA TEKNOHAMA

Serikali ya Tanzania imewatahadharisha wananchi kuzingatia matumizi sahihi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEKINOHAMA) ili kuondoa vitendo vya uhalifu hapa nchini.

Hayo yamesemwa na Kaimu Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano Serikalini Bi Prisca Ulomi wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es salaam.

Akifafanua Bi Prisca amesema kuwa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia kwa kutambua umuhimu wa TEKINOHAMA wameamua kuandaa muswada wa Sheria za Matumizi Sahihi na Salama ya Mtandao (Cyber Laws).

Akieleza zaidi Bi Prisca amesema kuwa Muswada wa sheria hizo ni pamoja na Muswada wa Sheria ya Kulinda Taarifa Binafsi (The Personal Data Protection Bill), Muswada wa Sheria ya Biashara ya Miamala ya Kielektroniki (Electronic Transaction Bill), na Muswada wa Sheria ya Kuzuia Uhalifu kwa njia ya Kompyuta na Mtandao (Computer and Cyber Crimes Bills).

“Sheria hizo zitasaidia kuimarisha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano hapa nchini kwa kudhibiti uhalifu kwa kutumia mitandao na kuwalinda watoto dhidi ya matumizi yasiyofaa ya mitandao”. alisema Bi Prisca.

Bi Prisca aliongeza kuwa serikali imetumia gharama kubwa kuweka miundombinu ya TEHAMA ambayo imesaidia kuboresha na kuharakisha utoaji wa huduma mbalimbali na kubainisha kuwa wapo baadhi ya watu wanatumia vibaya teknolojia hiyo, hivyo kuna umuhimu wa kuwepo sheria zitakazodhibiti uhalifu kupitia mitandao.

Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia imetoa rai kwa wananchi kujiepusha na matumizi mabaya ya mitandao na badala yake watumie vizuri mitandao hiyo kwa maendeleo yao na taifa kwa ujumla hali inayoweza kuathiri ukuaji wa sekta hiyo nchini.

Popular Posts

Labels