Saturday, April 5, 2014

TAHADHARI DHIDI YA UHALIFU UNAOFANYWA KUTUMIA SIMU ZA MKONONI

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), kwa kuzingatia kifungu 5 (b) na (e) cha Sheria ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania ya 2003 inatoa tahadhari kwa watumiaji wa huduma za mawasiliano, wananchi na umma kwa ujumla kujihadhari na utapeli unaofanywa kwa kutumia simu za mkononi na mtandao wa intaneti kama ifuatavyo:

1. Usimpe mtu yeyote usiyemfahamu vizuri simu yako au kadi yako ya simu ili atumie.

2. Usitoe maelezo yoyote kuhusu namba yako ya simu au taarifa za binafsi kwa mtu yeyote anayekupigia simu kutaka taarifa hizo.

3. Usijibu ujumbe wa simu unaohusiana na fedha zako hata kama namba iliyotuma unaifahamu.

4. Usitekeleze maagizo yoyote yanayohusu fedha kwa ujumbe wa maandishi hata kama yanatoka kwenye namba ya mtu unayemfahamu. Mpigie aliyekutumia ujumbe uzungumze naye.

5. Usitekeleze maagizo yoyote kutokana na ujumbe wa simu za mkononi unaokutaka kutuma fedha kutoka namba ambayo mtumiaji wake unamfahamu na ambao unakueleza kwamba simu yake ina hitilafu hivyo hawezi kuongea, usitekeleze maagizo hayo.


6. Ukipata ujumbe kwamba umepokea fedha kwa njia ya simu, mpigie aliyekutumia na usitoe pesa hizo hadi uthibitishe kwamba zimetumwa kwa nia njema.

7. Weka njia za kuthibitisha taarifa kabla ya kufanya miamala ya kifedha kutumia simu ya mkononi.

8. Ukipigiwa simu na mtu yeyote kuhusu masuala ya fedha, hata kama unadhani unamfahamu mtu huyo; mpigie tena kwa namba yake unayoijua ili kuhakikisha kwamba ni yeye.

9. Iwapo unafanya biashara ya huduma za simu hakikisha kwamba simu unayoitumia kwa miamala ya kifedha ni tofauti na unayotumia kwa shughuli nyingine na hakikisha simu hiyo haitumiwi na mtu mwingine

10. Tumia namba ya siri ambayo sio rahisi mtu mwingine kukisia.

11. Usitoe namba zako za siri unazotumia kwa huduma

12. Thibitisha na hakiki namba ya mtu unayemtumia pesa au salio kabla ya kutuma

13. Ukipoteza simu au laini yako ya simu toa taarifa kwa mtoa huduma wako na Polisi mara moja.

14. Ukifanyiwa uhalifu ambapo simu au mtandao umetumika kufanyia uhalifu huo hilo nikosa la jinai. Toa taarifa Polisi ili wahalifu wasakwe na wafikishwe kwenye vyombo vya sheria.

15. Usipopata ushirikiano wa kutosha kwa mtoa huduma wako katika kutatua taizo lako wasilisha malalamiko yako Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania. Unaweza kuwasilisha malalamiko kwa kutuandikia ( S.L.P 474 Dar Es Salaam); kufika ofisini makao makuu namba 20 Sam Nujoma Dar es Salaam au kwenye ofisi za Kanda na Zanzibar; kupiga simu ( namba 0784 558270 au 0784 558271) na kwa barua pepe ( malalamiko@tcra.go.tz au complaints@tcra.go.tz)


Imetolewa na: MKURUGENZI MKUU, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania

Popular Posts

Labels