Serikali ya Tanzania ipo katika hatua ya mwisho za kuandaa sheria ya kukabiliana na uhalifu wa kimtandao ambapo kwa sasa inajiandaa kuwasilisha muswaada wa sheria hiyo kwenye baraza la Mawaziri.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Sayansi na Teknolojia wa Tanzania Profesa Makame Mbarawa wakati akizungumza kwenye baraza la wafanyakazi wa Wizara hiyo.
Profesa Mbarawa amesema kuwa sheria tatu zinatarajia kutengenezwa kupitia mpango huo wa kukabiliana na uhalifu wa mitandao zitagusa maeneo muhimu yatakayotumia mitandao hususani huduma za fedha kwa mtandao
Ameitaja mikakati mingine inayofanywa na serikali katika kuboresha sekta ya mawasiliano na teknolojia kuwa ni pamoja na uwekezaji utaogharimu kiasi cha fedha shilingi ishirini na uendelezaji wa ujenzi wa mkongo wa taifa wa mawasiliano.
Aidha amewataka watumishi wa Wizara hiyo kujadili namna ya kuboresha utendaji kwenye wizara bila ya kuwa na vitengo vingi akiwataka kuunganisha idara zitakazoshabihiana katika utendaji bila kutanguliza maslahi binafsi.