Wiki moja kabla ya kusitishwa huduma za programu ya kompyuta (OS) ya,Windows XP April 8,mwaka huu imefahamika kuwa waathirika wakubwa watakuwa ni benki na taasisi za
fedha ambazo hutumia mfumo huo katika mashine za kutolea fedha (ATMs) Shirika la Microsoft limethibitisha kuwa benki ni miongoni mwa taasisi nyingi zitakazoathirika na mabadiliko hayo.
Baadhi
zimeanza kufanyia kazi tatizo hilo, ikiwamo benki moja ambayo jana
alasiri ilituma ujumbe kwa wateja wake kuwa, “Ndugu mteja, kuanzia
Jumamosi saa 2:00 usiku Aprili 5, mpaka Jumapili saa 12:00 asubuhi
tutakuwa tunaboresha mashine zetu za ATM, hivyo kadi yako haitafanya
kazi kwa kipindi hiki. Asante.”
Kwa mujibu
wa Microsoft asilimia kubwa ya benki katika nchi zinazoendelea zinatumia
programu ya Windows XP katika kuendesha ATM, hivyo kuwa moja ya
waathirika wa mpango huo.
Katikati
ya Machi, Microsoft ilitangaza kusitisha huduma zote zinazohusiana na
bidhaa zake za Windows Xp kufikia Aprili 8, mwaka huu. Pia shirika hilo
litasitisha ufanisi wa programu ya kuzuia na kupambana na virusi ya
Microsft security Essentials katika mfumo wa Windows Xp, hivyo kufanya urahisi wa kompyuta zinazoitumia kukosa ulinzi.
Mkurugenzi
wa Kampuni ya Twiga Hosting, Jacob Urassa alisema Watanzania hawatakiwi
kupuuza onyo hilo kwa kuwa ikifika Aprili 9 usalama wa taarifa zao
utakuwa hatarini.
“Windows XP ni dhaifu mara tano
zaidi ya Windows 7 na 8, kwa hiyo Microsoft wameona ni bora wakaitoa
sokoni. Kwa maana hiyo ATM na kompyuta zote zinazotumia programu hizo
hazitakuwa na ulinzi wa uhakika,” alisema Urassa ambaye ni mtaalamu wa
masuala ya Teknolojia ya Mawasiliano (IT).
Alisema kuwa
kuna idadi kubwa sana ya Watanzania wanaoendelea kutumia bidhaa hizo
zikiwemo taasisi kubwa nchini hivyo kuna haja kubwa ya kuchukua hatua za
kubadilika na teknolojia.
Naye, Ofisa
Uhusiano wa Benki ya Posta, Noves Moses aliwatoa wasiwasi wateja wake
kuwa licha ya kusitishwa kwa matumizi ya Windows XP, bado benki hiyo
itaendelea kutoa huduma zenye kiwango kile kile.
Chanzo - Mwananchi