Baraza la Sanaa la Taifa nchini Tanzania (BASATA) limetoa
siku saba kwa wasanii,vituo vya radio,runinga wamiliki wa tovuti na wale wenye wasifu kwenye mitandao
ya kijamii kuondoa nyimbo zote au maudhui yenye muelekeo unaoenda kinyume na
maadili, matusi na kashfa mbalimbali.
Taarifa ya BASATA iliyotiwa
saini na Katibu Mtendaji wa Baraza hilo Godfrey Mngereza imevitaka pia vyombo vya habari zikiwemo radio na
luninga kuondoa na kuacha mara moja kucheza au kurusha nyimbo zote zenye maudhui
hayo.
Mngereza amesema maudhui ya
kashfa,matusi,kejeli,udhalilishaji zinatishia kuigawa jamii ya watanzania
katika kipindi hiki ambacho taifa linaendelea na kampeni za kujiandaa na
uchaguzi mkuu tarehe 25 mwezi wa kumi mwaka huu.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa kifungu namba 118 [a-d]
cha sheria ya bunge namba 9 ya mawasiliano ya mtandao ya mwaka 2010 vinaelekeza
kuwa ni marufuku kwa njia yoyote kwa mtu au chombo chochote kutengeneza ujumbe
ambao unamlengo wa matusi ,dharau,uzushi au jinai kwa lengo la kutukana
,kutisha, kusumbua au kushusha hadhi
ya mtu mwingine.