Tuesday, May 24, 2016

UfUNGWAJI WA SIMU BANDIA JUNI 16, 2016

Hadi kufikia juni 16 mwaka 2016 , Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) itakua imeshafunga simu nyingi bandia pamoja na vifaa vingine vya mawasiliano ambavyo havikidhi viwango na mahitaji ya soko la tanzania . Kama mtanzania kuna mambo kadhaa unatakiwa kujua kuhusu simu bandia na  vifaa vya mawasiliano

Simu zote na vifaa vyake wakati vinatengenezwa mpaka kupitishwa kutumiwa huwa vinapitia katika taratibu kadhaa zinazohusu ubora na mahitaji ya kibinadamu ambayo hayaleti madhara yoyote kwa afya na mazingira . Simu bandia hazipitii utaratibu huu wala ukaguzi na wala hazijulikani watengenezaji wake wala zilipotoka ili kufuatilia . matokeo yake zinaweza kuleta athari za kiafya na mazingira kama nilivyosema hapo awali .

Kama simu itakuletea madhara ya kiafya ina maana utatumia muda na gharama nyingi kujipatia matibabu yaliyotokana na madhara kadha wa kadha hapo sio kila mtu ana uwezo wa kugharamia au kugharamiwa , kama ulikua umajiajiri basi biashara au mengine yanaweza kufa kwa sababu ya matibabu na mengine lakini ungekua na kifaa kizuri shida hii usingeweza kuipata kwa sababu ingekua na viwango vya kutosha .

Hapo pia kuna suala la kupeleka simu kwa fundi mara kwa mara kwa sababu ya ubovu au mengine ambayo simu haiwezi kufanya kutokana na viwango vyake havifu kwa mwananchi wa kawaida hii pigo kwake , wengine wanaweza kuamua kununua nyingine tu maana gharama zake pia ni nafuu kulinganisha na zile halisi zenye vitu vinavyolingana .

Simu bandia na vifaa vyake huingizwa nchini kupitia njia za panya maana kama zikikaguliwa zitagundulika na kuharibiwa na wahusika kufikishwa katika vyombo vya sheria , hii ina maana serikali ina kosa mapato kutokana na kodi , ajira zinapungua na huduma nyingine zinakosekana kutokana na hujuma kama hii .

Kumbuka kwamba wauzaji wote wa vifaa vya mawasiliano kama simu husajiliwa TCRA ambapo ada yake kwa mwaka ni laki 5 kwahiyo huwa na kibali Fulani , kama mtu hana kibali cha kuuza vifaa hivi maana yake unatakiwa kuwa na mashaka nae ni vizuri ukafikisha taarifa kwa mamlaka ya mawasiliano haraka ili hatua kuchukuliwa .

Kiusalama wa kawaida pia matumizi ya simu bandia na vifaa vyake yanaweza kuleta mambo mengi mfano ni suala la wizi wa mtandao kwa kuwa simu inakua haina mfumo mzuri na wa uhakika wa kujilinda na kwa hizi za kisasa hata antivirus na nyingine hautaweza kuweka , mhalifu anaweza kuingilia kwa urahisi hata kutokea maeneo mengine .

Kuna tukio lilitokea Saudi Arabia mwaka jana ambapo gaidi alifanikiwa kuingia katika kambi ya polisi akajitoa mhanga na kuua wengine 30 . katika tukio hili iligundulika kwamba gaidi huyu na mtandao wake walikua wanatumia simu bandia na kujisajili line kutumia majina ambayo sio yao na matokeo yake ni kufanikiwa kupita vizuizi vyote mpaka eneo nyeti la kambi ya polisi .

Kuanzia tukio hilo Serikali ya Saudi Arabia ilitoa tangazo la kufungwa wauzaji wote wa simu bandia na laini zisizosajiliwa .
Tukio kama la Saudi Arabia linaweza kutokea hata Tanzania na maeneo mengine mengi kama matumizi ya simu bandia na vifaa vyake yakiendelea bila kikomo .

Mwanzo wa Mwaka 2016 , Benki moja maarufu ilitaka kuibiwa milioni 900 kwa njia ya mtandao baada ya kununua kifaa bandia cha mawasiliano ya kiofisi , wahalifu walitumia kifaa hiko kuingilia akaunti za benki ili kuhamisha fedha ila kuna vitu walikwama na miongoni ni ujuzi wao katika matumizi ya Lugha lakini suala ni ununuzi wa kifaa bandia cha mawasiliano .

Pia suala la Ushindani wa kibiashara na Ubinifu hupotea na kufa kabisa katika maeneo ambayo biashara za vitu bandia hushamiri , mtu mwenye simu bandia ya Nokia 200 kwa mfano atauza shilingi 4 wakati ile halisi ni 8 hii ina maana baada ya muda mfupi Yule wa 8 anaweza kufunga biashara yake na kufuta wafanyakazi waliobuni kifaa husika , kukijaribu , kukitafutia masoko na mengine mengi . sasa muwekezaji hatapenda kuwekeza Tanzania akijua kuna soko kubwa la vitu bandia .

Kama unafanya kazi zako kutumia simu , ukiwa na simu bandia utaweza kuona ubora  wa picha , sauti , cover , kioo na vitu vingine unavyokua mbaya kulinganisha na vile vilivyoko katika simu original yenye ubora wa uhakika . kwahiyo utaweza kukosa kazi kwa kuharibu kazi kwa kutumia vifaa bandia visivyokidhi mahitaji .

Suala la vitu bandia liko katika vitu vingi tu ambavyo tunajua madhara yake kama spea za magari ambazo huchangia katika ajali za mara kwa mara , vifaa vya ujenzi ambavyo huchangia majengo kuporomoka au kuwaka moto .

Vita dhidi ya vifaa bandia viko dunia nzima , sio Tanzania tu , kwahiyo tuunge mkono jitihada hizi za serikali chini ya TCRA , POLISI , TBS na mamlaka nyingine zenye uwezo huo kisheria ili kulinda nchi na watu wake .

Mwandishi wa makala hii hana uhusiano na kampuni yoyote ya simu wala mamlaka ya mawasiliano tanzania . Ulichomaliza kusoma ni kwa ajili ya kujifunza ili kuelimika kisha usaidie wengine .
YONA FARES MARO
0786 806028

Popular Posts

Labels