Friday, April 5, 2019

UCHUNGUZI WAONESHA TATIZO LA KIMFUMO LILISABABISHA AJALI YA BOEING 737 MAX 8

 Image may contain: aeroplane

Ripoti ya awali ya uchunguzi wa ajali ya ndege la Shirika la Ndege la Ethiopia safari namba 302 inaonyesha kwamba ajali hiyo ilitokana na tatizo la kimfumo katika ndege na kwamba marubani wa ndege hiyo walifanya kila walichoelekezwa na kufuata taratibu zote kwa mujibu wa watengenezaji wa ndege hiyo lakini hawakufanikiwa kuizuia isianguke.

Mfumo katika aina ya ndege iliyoanguka (Boeing 737 Max 8 ) umekuwa katika mjadala mkubwa kiasi cha kusababisha nchi nyimgi kuamrisha kusimamishwa kwa matumizi ya ndege hizo na Wizara ya Sheria, Mkaguzi Mkuu masuala ya Usafirishaji na Kamati za Bunge la Marekani vimeanzisha uchunguzi tofauti na maalum wa namna ambavyo kampuni hiyo ilivyofanya maboresho ya mfumo na walivyopata kibali cha uthibitisho wa ubora toka Mamlaka ya Anga ya Marekani.


Ndege hiyo iliyoanguka Machi 10, 2019 na kuua abiria wote 157, ilikuwa ni ya pili ya aina hiyo kuanguka ndani ya miezi 5 na hilo likazua hofu kwa wasafiri na wasafirishaji kuhusu usalama wa ndege hizo.


Ripoti kamili inatarajiwa kutoka baadae sana, lakini punde nitakapopata nakala ya awali ya ripoti hiyo nitaileta hapa ili kushiriki nanyi juu ya dondoo za uchunguzi huo.


Shirika la Boeing linalotengeneza ndege hizo lilitangaza kwamba lingefanya maboresho ya mfumo huo hivi karibuni lakini inaonekana wamesubiri matokeo haya ili kuhakikisha wanawathibitishia wateja wake kuwa wanaboresha kile kinachowatia hofu kutokana na ajali mbili za ndege zake.

Na: Mubelwa Bandio-Marekani

Popular Posts

Labels